Mgombea wa urais wa UDA, William Ruto amezuru maeneo yenye ufuasi wake mkubwa ili kuwapigia debe wagombea wa UDA ambao wanaonekana kupata ushindani mkali kutoka kwa wagombea huru.
Ziara ya Ruto ilianzia Nandi Hills, kisha Kesses na Moiben katika Kaunti ya Uansin Ngishu, Tot na Iten huko Elgeiyo Marakwet.
Ruto na viongozi walioandamana naye wamewataka wakazi kuwaunga mkono wagombea wa UDA katika uchaguzi wa tarehe tisa mwezi Agosti.
Kando na hilo, Ruto amemtaka mshindani wake katika kinyang’anyiro cha urais, Raila Odinga wa Azimio kuhudhuria mjadala wa urais ambao umeratibiwa kufanyika Jumanne tarehe 26.
Akizungumza katika Eneo Bunge la Kesses, Ruto amesema yuko tayari kumkabili Odinga wakati wa mdahalo huo na kumsihi kutoogopa kuwahuhuria.
Kauli yake imetiliwa mkazo na Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro ambaye amesema Odinga ameingiwa na wasiwasi.
Kamati ya Kampeni za Raila Odinga ilisema kiongozi huyo wa ODM hatashiriki mjadala katika jukwaa moja na Ruto na kwamba Ruto hana maadili ya kimsingi kushiriki mazungumzo na Raila kuhusu masuala ya uongozi, ufisadi na maendeleo.
Discussion about this post